
Mwj. Ezra Mbenanga
29. Juni 2025
Konde Marathon, Iliyofanyika tarehe 28 June 2025, ili kuchangisha fedha za kununulia vifaa tiba katika hospitali mpya ya kanisa inayoitwa Konde Hospital and Diakonia Center.
Mbeya, Juni 28, 2025
Mji wa Mbeya ulishuhudia tukio kubwa la kihistoria baada ya kufanyika kwa mara ya kwanza mbio za Konde Marathon 2025, zilizokuwa na malengo makuu ya kuchangisha fedha kwa ajili ya kusaidia huduma za afya kupitia Hospitali ya Konde na Kituo cha Udiakonia kilichopo Sae, jijini Mbeya.
Marathon hii, iliyoandaliwa na kampuni ya Konde Sports Promotion Co. Ltd kwa kushirikiana na KKKT Dayosisi ya Konde, iliwakutanisha washiriki wa rika na makundi mbalimbali kutoka ndani na nje ya nchi. Washiriki walishiriki katika viwango tofauti vya mbio: kilomita 21, kilomita 10, kilomita 5 na kilomita 2, ambapo mbio za watoto na watu wenye ulemavu zilipata mwitikio wa pekee kutoka kwa jamii.
Kwa mujibu wa waandaaji, zaidi ya washiriki 800 walijisajili kushiriki katika tukio hili. Aidha, huduma za macho zilizoambatana na marathon hii ziliwanufaisha wananchi zaidi ya 400, waliopimwa afya za macho na wengine kupata msaada wa miwani na matibabu ya awali.
Akizungumza katika tukio hilo, Askofu wa KKKT Dayosisi ya Konde, Mhashamu Geoffrey Samuel Mwakihaba, alisema kuwa mbio hizi hazikuwa za michezo pekee bali pia ni ishara ya mshikamano na mshirikiano wa kijamii kwa ajili ya kuunga mkono afya na ustawi wa wananchi. “Kupitia Konde Marathon, tumejifunza kuwa mshikamano wa jamii unaweza kuwa daraja la kuleta matumaini na maisha bora kwa kila mtu,” alisema Askofu.
Viongozi wa serikali, chama cha riadha mkoa, pamoja na wadau mbalimbali walihudhuria na kushiriki katika maandalizi na kufanikisha mbio hizo. Usalama ulidumishwa kwa msaada wa polisi, timu za afya na maelfu ya mashabiki waliokusanyika kuunga mkono washiriki.
Washindi wa mbio walituzwa zawadi mbalimbali kwa mujibu wa viwango vya mbio walivyoshiriki, huku zawadi kubwa kwa washindi wa kilomita 21 ikifikia hadi Tsh. 800,000/=.
Konde Marathon 2025 imeacha alama ya pekee katika historia ya michezo mkoani Mbeya, na waandaaji wameahidi kuendelea na mbio hizi kila mwaka, kwa malengo mbalimbali ya kijamii na kiroho.